MKUTANO WA 49 WA KAMATI YA KITAIFA YA UWEZESHAJI NA URAHISISHAJI WA USAFIRI WA ANGA NCHINI WAFANYIKA ZANZIBAR
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe.Rahma Kassim Ali (katikati),Mkurugenzi Mkuu wa TCAA na wanakamati ya kitaifa ya uwezeshaji na urahisishaji wa usafiri wa anga nchini kwenye picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa mkutano wa 49 wa kamati hiyo.
Kamati ya kitaifa ya uwezeshaji na urahisishaji wa usafiri wa anga nchi imekutana katika mkutano wa 49 wa kamati hiyo uliofanyika mjini Unguja visiwani Zanzibar na kupata baraka za ufunguzi kutoka kwa waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe.Rahma Kassim Ali.
Akizungumza wakati wa hotuba yake,Mhe.Rahma Kassim Ali aliwahimiza wajumbe wa kamati hiyo kufanya kazi kwa bidii na kutanguliza uzalendo katika kutafuta suluhu na kujadili namna ya kutatua changamoto zinazokabili sekta ya usafiri wa anga kwani ni chanzo muhimu cha mapato ya nchi.
“Nashukuru kwa mualiko wa ufunguzi wa mkutano huu muhimu sana unaokutanisha wadau wa usafiri wa anga nchini.Nina imani kubwa kuwa utakwenda kuwa na tija zaidi katika kupunguza na kutatua changamoto mbalimbali na bila shaka kuimarisha uchumi wa taifa letu”, ameeleza Mhe.Rahma Kassim Ali
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA) Bw.Hamza S. Johari akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa 49 kamati ya kitaifa ya uwezeshaji na urahisishaji wa usafiri wa anga nchini
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA) Bw.Hamza S. Johari amesema kamati hii imejikita zaidi katika utekelezaji wa sheria na mkataba wa usafiri wa anga wa kimataifa maarufu kama mkataba wa Chicago wa mwaka 1944 unaotaka katika masuala ya abiria na mizigo wanapopita katika uwanja wa ndege kuwe na urahisi, usalama, ufanisi na kwa haraka bila ya kuwa na ucheleweshaji sana kwa abiria na mizigo pasipo kuwa na sababu za msingi.
“Lengo kubwa la mkutano huu ni kuziangalia changamoto zinazoleta uchelewashaji kwa abiria na mizigo katika viwanja vyetu vya ndege na kuja na hatua zitakazo leta urahisi na faraja kwa abiria wanaotumia usafiri wa anga nchini”, amefafanua Bw. Johari
Sambamba na hilo Bw. Johari amesisitiza kuwa usafiri wa anga hauruhusu upitishaji wa vitu haramu kama vile madawa ya kulevya na kwamaana hiyo inawahusisha na kushirikiana na wadau wote wanaohusika ili kuhakikisha hilo linafanyika ili kuendelea kuilinda taswira ya nchi yetu.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw.Daniel N. Malanga amesema kuwa mkutano huu unatoa fursa ya kipekee kwa wadau wa sekta ya usafiri wa anga nchini kukutana pamoja kujitathini, kujadiliana na kuja na mapendekezo yatakayoenda kuleta maboresho, unafuu na kuimarisha sekta ya anga hapa nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uwezeshaji na Urahisishaji wa Usafiri wa Anga nchini,Bw.Daniel N. Malanga akitoa neno la ukaribisho kwa waliohudhuria mkutano wa 49 kamati ya kitaifa ya uwezeshaji na urahisishaji wa usafiri wa anga nchini
“Kamati hii ni mtambuka hivyo inatoa fursa ya kujadili changamoto mbalimbali kwa upana kwani inajumuisha wadau mbalimbali wa usafiri wa anga nchini. Kwahiyo katika mkutano huu tutajadili kwa kina changamoto zinazokikabili kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA)”, amesisitiza Bw. Malanga
Katika hatua nyingine, kamati imefanya ziara katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar (AAKIA) na kujionea namna shughuli zinavyofanyika kwenye jengo la pili la abiria (Terminal 2).
Aidha, pamoja na hayo kamati imetembelea jengo jipya la abiria (Terminal 3) ambalo linatarajia kuanza kuhudumia wasafiri ifikapo Julai Mosi mwaka huu.
Vilevile, pamoja na changamoto walizozibaini kamati imeipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua iliyofikia katika ujenzi wa jengo hilo la abiria linalotarajia kuhudumia makadirio ya abiria milioni moja na nusu kwa mwaka.
Mkutano huu unafanyika mara mbili kwa mwaka na unahusisha wadau wa usafiri wa anga wakiwemo Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA),Mamlaka za Viwanja vya Ndege (TAA na ZAA),Idara za Kiusalama katika viwanja vya ndege,wadau wa mazingira na watoa huduma kwenye viwanja vya ndege nchini.
Kwa mwaka huu, mkutano umefanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 27 hadi 28 Mei, 2021.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjjI4sLtQ31Nkato76vhOS2eAIgPBCxEZT0Ze-lGIgBPr8ytXdkwRFr2WeGzFZFKYTfMh1grDh6zFsJYg_70Pgtte8mOgBpBkXqzBGLCqThNQxkrlbVM4tM6hC8MdFW_SDPtFz4ny98YjE/w640-h396/1.jpg)
Safii
ReplyDelete